4 Februari 2015 - 18:58

Katika wakati huo huo Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema nchi hiyo haina mpango wa kupeleka silaha Ukraine kupambana na wapiganaji wanaoiunga mkono Urusi katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Shambulio la kombora dhidi ya hospitali mashariki  mwa  Ukraine limesababisha  watu  wanne  kuuwawa leo, wakati waziri wa mambo ya kigeni  wa  Marekani  akitarajiwa  kufanya  ziara  mjini  Kiev ziara ambayo huenda suala la kuipatia silaha  nchi  hiyo  likawa  juu  katika ajenda  za  mazungumzo.

Vifo  hivyo vimetokea  wakati  mbinyo  wa  jumuiya  ya  kimataifa kusitisha  mapigano  unaongezeka  ambapo kumeshuhudiwa  mamia ya  raia  wakiuwawa  katika  wiki  za  hivi  karibuni  wakati  waasi wanaoiunga  mkono  Urusi  wakisonga  mbele  katika  maeneo yanayoshikiliwa  na  serikali.

Uwanja wa kuchezea  watoto pia ulishambuliwa, mkaazi  wa eneo hilo ameliambia  shirika  la  habari la AFP, na  maafisa  wa  serikali wamesema  raia  wengine  wanane wameuwawa  katika  mapigano katika  jimbo  hilo  katika  muda  wa  saa  24  zilizopita.

Wakati idadi ya vifo inazidi kupanda mkuu  wa  masuala  ya  kigeni wa  Umoja  wa  Ulaya  Federica Mogherini ametoa wito wa kusitisha mapigano mara  moja  kuruhusu  raia  kuondoka  katika  eneo  la mapigano.

 Katika wakati huo huo Waziri  wa  ulinzi   wa   Ufaransa  Jean-Yves  Le Drian  amesema nchi  hiyo haina  mpango  wa  kupeleka  silaha  Ukraine  kupambana na  wapiganaji  wanaoiunga  mkono  Urusi  katika  eneo  la mashariki  mwa  nchi  hiyo.

Le Drian  amesema  hayo  akizungumzia  kuhusu  mjadala uliozushwa  na  ripoti  kuwa  Marekani  inatafakari  kuipatia  Ukraine silaha.  Le Drian  amesema  msimamo  wa  Urusi  wa  kuwapatia msaada  wapiganaji  wanaotaka  kujitenga  nchini  Ukraine haukubaliki,  na  amesema  mataifa  ya  Ulaya  yanaendelea  na vikwazo  kutokana  na  hatua  hiyo.

 Makubaliano  ya  kusitisha  mapigano  kati  ya  waasi  na  Ukraine yamevunjika  katika  mwezi  uliopita, na  mapambano  mapya   ya wapiganaji  yanaendelea  dhidi  ya  maeneo  muhimu  ya mawasiliano  na  usafiri  mashariki  mwa  Ukraine.